CCM; PINDA NA HAWA GHASIA WANG'OKE
CCM; PINDA NA HAWA GHASIA WANG'OKE
Rais Jakaya Kikwete, ameshauriwa kumng’oa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ikielezwa sababu kuwa ndiye kikwazo katika utendaji wa Serikali na kwamba akiachwa ataipeleka pabaya Serikali na CCM.
Kikwete pia ameshauriwa kumfukuza kazi Waziri wa
Tamisemi, Hawa Ghasia, kwa kushindwa kukabiliana na matatizo ya
ubadhirifu katika halmashauri nchini.
“Kama (Rais) unaitakia mema nchi na CCM kuchukua
hatua za kuwafukuza kazi Pinda na Waziri Ghasia,” alisema Mbunge wa
Mwibara, Khangi Lugola (CCM), juzi alipochangia taarifa za Kamati za
Bunge kuhusu hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30
mwaka jana.
“Kwa nini Watanzania wafe kwa kunyimwa misaada na
wafadhili kwa sababu ya mtu mmoja tu Pinda, kwa ajili ya Ghasia
ameiendesha Tamisemi kama Saccos ama Vikoba?” alihoji.
“Mchawi wetu ... ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda
amekuwa mpole mno hawajibiki,” alisema Mh. Lugola na kuongeza, “Kuanzia
jana (juzi) Waziri Mkuu anahudhuria mahafali.”
Wakati Lugola akizungumza mawaziri waliokuwepo bungeni ni wanne, manaibu mawaziri wawiliwawili, wakati mawaziri wote 53.
India, Ufaransa, Marekani, Canada zaomboleza kipekee
Wakati Bara la Afrika likiendelea na maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa kwanza wa Afrika Kusini na mkombozi aliyepinga siasa za ubaguzi za makaburu, Nelson Mandela, mataifa mengine duniani yameonyesha kufanya maombelezo katika namna mbalimbali.
Pamoja na kutuma salamu za rambirambi kwa
familia ya Mandela na wananchi wa Afrika Kusini, viongozi wa mataifa
makubwa duniani wameonyesha kuguswa na msiba huo kiasi cha kuomboleza
kwa namna tofauti tofauti.
India
Hii inaweza kuwa ni nchi mojawapo ambayo
imetangaza siku nyingi zaidi za maombolezo kwa ajili ya kifo cha Nelson
Mandela kutoka nje ya Bara la Afrika.
Baada ya kupata taarifa za kifo cha Mandela,
Serikali ya India kupitia Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Manmohan Singh
aliwatangazia siku tano za maombelezo na kuamuru bendera zipeperushwe
nusu mlingoti katika kipindi hicho cha maombolezo.
Sambamba na hilo, Singh alimwelezea namna kiongozi huyo wa Afrika alivyokuwa shujaa katika kupinga mfumo wa kibaguzi.
Ufaransa
Kuonyesha kuwa taifa hili pia limeguswa kwa kiasi
kikubwa na msiba huu, jengo refu zaidi mjini Paris la Eiffel Tower
liliwashwa taa zenye rangi zilizopo kwenye Bendera ya Afrika Kusini.
Picha zilizopigwa katika jengo hilo mpaka siku ya
jana, linaionyesha likiwa limenakshiwa na taa zenye rangi tano za
bendera hiyo zikiwemo nyekundu, kijani, nyeusi, njano na nyeupe.
Marekani
Taifa hili lenye nguvu duniani limeonyesha heshima
kubwa kwa Nelson Mandela kwa kupeperusha bendera zake nusu mlingoti
nchi nzima na kuweka siku tatu za maombolezo.
Kana kwamba hiyo haitoshi taa zenye rangi ya
Bendera ya Afrika Kusini zilionekana kung’arisha jengo la Empire state
lililopo NewYork na Hoteli ya Omni iliyopo Dallas.
Mjini Washington jengo la Ubalozi wa Afrika Kusini lilitawaliwa
na taa hizo pamoja na bendera za nchi hiyo hali iliyosababisha mwonekano
wa eneo hilo kubadilika kabisa.
Pia kiongozi wa taifa hilo Rais Barack Obama alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Graca Machel ambaye ni mjane wa Mandela.
Taarifa kutoka Ikulu ya Marekani ilisema kuwa Obama alimpigia simu mama Machel kwa lengo la kumtumia salama za rambirambi.
Canada
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya
habari nchini Canada, Waziri Mkuu Stephen Harper amewaalika mawaziri
wakuu wengine wastaafu wa nchi hiyo kuungana naye kuelekea Afrika Kusini
kwa ajili ya mazishi ya Nelson Mandela.
Australia na Uingereza
Kama ilivyo kwa nchi nyingine, mataifa haya pia
yalitangaza siku za maombolezo sanjari na kupeperusha bendera zake nusu
mlingoti kuashiria maombolezo ya kifo cha kiongozi shujaa na mahiri
barani Afrika, hayati Nelson Mandela.
Stars kuivaa Kenya nusu fainali
Mombasa. Ushujaa wa kipa namba moja wa Kilimanjaro Stars, Ivo Mapunda umeivua ubingwa Uganda na kuiingiza Stars nusu fainali ya Kombe la Chalenji.
Stars itacheza na Kenya iliyoilaza Rwanda bao 1-0
katika mechi nyingine ya robo fainali iliyochezwa jana jioni kwenye
Uwanja huohuo wa Manispaa unaobeba mashabiki 15000.
Uganda iliutwaa ubingwa huo mwaka jana mjini
Kampala ikiwa haijafungwa bao hata moja kwenye mechi zake zote, Uganda
ilikuwa inaelekea kutimiza rekodi hiyo lakini jana Stars ikatibua mambo.
Awali kwenye mechi za makundi Uganda ilikuwa haijaruhusu bao lolote.
Mapunda anayeichezea Gor Mahia ya Kenya alipangua
penalti mbili za Uganda ambayo kocha wake, Sredejovic Milutin ‘Micho’
alijitetea kwamba penalti hazina ufundi na wala Stars haijafanya cha
ajabu. “Hakuna cha ajabu kwenye penalti, hakuna fundi.”
Licha mwamuzi Msomali, Wish Wabarow kuonekana
kuzidiwa na mchezo, mechi hiyo ilimalizika kipindi cha kwanza Stars
ikiongoza mabao 2-1 huku ikishangiliwa na uwanja mzima uliokuwa
umetawaliwa na Wakenya na Watanzania walioingia kupitia Lungalunga,
Tanga.
Straika wa Uganda anayewindwa na Yanga, Danny
Serunkuma ndiye aliyefunga bao la kwanza dakika ya 16 akipiga shuti kali
katikati ya mabeki wa Stars lakini dakika mbili baadaye Mrisho Ngassa
alisawazisha kwa shuti kali kutoka nje kidogo ya boksi likamshinda kipa
Benjamin Ochan.
Ngassa huyohuyo akapiga bao la pili kwenye eneo
lilelile dakika ya 38. Mchezo huo uligubikwa na aibu ya aina yake
kutokana na kutokuwepo kwa wasaidizi wa Msalaba Mwekundu kwa kile
kilichodaiwa kwamba hawajalipwa chao na Cecafa.
Timu hizo zilishambuliana kwa kasi kipindi cha
kwanza ambapo mastraika Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu waliipa shida
Uganda ambayo kwa siku ya jana straika wake, Danny Serunkuma ndiye
aliyeisumbua zaidi Stars.
Kipindi cha pili dakika 52 Aboubakar Salum ‘Sure
boy’ ambaye alikuwa akichezesha timu, alionyeshwa kadi nyekundu baada ya
kumkanyaga beki wa kushoto wa Uganda, Godfrey Walusimbi.
Dakika ya 75 beki mrefu wa Uganda alifunga bao laini baada ya Ivo kuutema mpira wa kona ya Wakiro Wadada.
Baada ya kumalizika kwa dakika 90, zilipigwa
penalti ambapo Uganda ilikosa tatu na Stars ikakosa mbili. Penalti za
Stars zilipigwa na Erasto Nyoni na Mbwana Samatta (walikosa), Amri
Kiemba, Athuman Idd na Kelvin Yondani. Uganda walipiga Danny Walusimbi
(alikosa), Emanuel Okwi, Aucho Khalid (alikosa), Hamis Kiiza na
Serunkuma aliyekosa penati ya mwisho na kuivusha Stars.
Ivo Mapunda ambaye alikuwa akishangiliwa na
mashabiki wengi wa Kenya alisema: “Siamini kwamba tumeshinda, ni Mungu
tu. Mpira ulikuwa mgumu sana na tulicheza na timu ngumu ambayo tumeitoa
kwa juhudi binafsi za wachezaji.”
Jela ilivyokuwa ‘Chuo Kikuu’ cha Mandela
Juni 12, 1964, Nelson Mandela alihukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kufanya hujuma dhidi ya Serikali ya kibaguzi ya Makaburu.
Hata hivyo Mandela alitumikia kifungo hicho kwa
miaka 27 na kutoka akiwa mtu aliyebadilika kitabia, akiwa mtulivu, akiwa
na hekima, mwenye busara na mwenye kuheshimika katika jamii.
Mandela alianza kutumikia kifungo katika jela
iliyopo kwenye kisiwa cha Robben kilichopo kwenye bahari ya Atlantic
umbali wa kilometa 12 kutoka mji wa Cape Town, alimotumikia kifungo kwa
miaka 18, na mwaka 1982 aliondolewa ndani ya kisiwa hicho na kuhamishiwa
kwenye gereza pia lenye ulinzi mkali la Pollsmoor lililopo Cape Town na
siku chache kabla ya kuachiwa huru alihamishiwa gereza lililopo mjini
Cape Town la Victor Verster.
Kisiwa cha Robben kwa takriban miaka 400 iliyopita
kimekuwa kikitumika kama eneo la kuadhibu watu, kuweka watu katika
maisha ya kuwatenga na kuwafunga jela. Ni kisiwa kwa ajili ya watu
wasumbufu wa kisiasa, wasumbufu katika jamii na watu wasiotakiwa katika
jamii.
Kama ilivyo kwa viongozi na wanaharakati wengine
wa ukombozi wa kiafrika waliopata changamoto za Serikali za kikoloni kwa
kukamatwa, ambao baadaye walikuja kushika uongozi wa nchi zao, kama
vile Kwame Nkrumah wa Ghana, Jomo Kenyatta wa Kenya na Robert Mugabe wa
Zimbabwe, Mandela naye alipotoka jela alikuwa Rais wa kwanza mweusi
nchini Afrika Kusini.
Gereza la Kisiwa cha Robben, lililofahamika kwa
jina la gereza ndani ya gereza, lilikuwa ni gereza lenye zahama na
ukiwa. Kufungwa ndani ya gereza hilo maana yake ni muda mwingi kufanya
kazi za suluba, lakini kulikuwa na fursa kwa mfungwa kupata muda wa
kujisomea, kufanya mijadala na kujipima. Miongoni mwa masharti ya
kushikilia maadili ndani ya gereza hilo ni kwa wafungwa kujikita kwenye
kusoma na kufanya mijadala. Tabia ya Mandela na uongozi wenye weledi ni
matokeo ya maisha ya jela au ‘Chuo Kikuu cha Kisiwa cha Robben.’
“Hakuna zaidi ya kuelekeza akili zako kwa kuwa
mtulivu zaidi kwa kukubali ukweli wa jamii yako,” alisema Mandela.
Mwanzoni mwa mwaka 1972, alipewa ofa ya kutoka jela kwa sharti la
kutangaza kukomesha vurugu dhidi ya Serikali ya Makaburu, ofa mabayo
aliikataa akisema kuwa Serikali ndiyo imekifanya chama cha ANC kutumia
njia ya uanaharakati.
Maisha ya jela ndiyo yaliyombadili Mandela na kuwa
kiongozi mwenye ushawishi, ambapo akiwa gerezani alijifunza kuhusu
hisia za binadamu na namna ya kuondoa hofu na mambo yasiyo ya usalama
kwa wengine. Akiwa gerezani Mandela aliwavutia askari magereza kwa namna
alivyokuwa mtetezi wa haki, mweye heshima na mwenye uelewa wa masuala
ya kisheria, ambapo ndani ya gereza la Kisiwa cha Robben alikuwa
kiongozi wa wafungwa wenzake.
Kwa mujibu wa taarifa askari magereza walikuwa chini ya uongozi wa wafungwa na wafungwa walikuwa chini ya uongozi wa Mandela.
Mwandishi wa habari Eddie Koch aliandika kwenye
magazeti ya Mail na Guardian kuwa selo namba saba alimokuwa akiishi
Mandela, lilikuwa eneo lenye harakati nyingi za ulinzi mkali ndani ya
gereza hilo kwa kila Jumamosi ya wiki.
Wakati Mandela akiwa ndani ya gereza hilo kulikuwa
na mikwaruzano ya wafungwa, kutoka kitengo cha kijeshi cha ANC, chama
cha Pan Africanist Congress na wanaharakati wa Steve Biko’s Black.
Vurugu ndani ya gereza hilo zilifanyika kwa misingi ya kupingana watu
binafsi na tofauti ya itikadi, ambapo vurugu hizo zilikuwa kipimo cha
mbinu za uongozi wa kidiplomasia wa Mandela na wenzake.
Taarifa zilisema wafungwa wengi wapya walipelekwa
kwenye gereza hilo la Kisiwa cha Robben, kama vile viongozi wa wanafunzi
wa Soweto, wawakilishi wa baraza waliochochea vijana hadi wakaazisha
vurugu nchini humo mwaka 1976, hawakuwa na ufahamu kuhusu hali ya
kisiasa ndani ya gereza hilo.
Hivyo ilikuwa ni jukumu la Mandela na wenzake kuwaelimisha na
kuwapa taratibu za gereza hilo wafungwa hao wapya vijana, gereza hilo
lilikuwa sehemu huru kwa wasomi kutumia vipaji vyao. Gereza la Kisiwa la
Robben lilijengwa kwa namna ambayo limezuia mawasiliano kati ya
uongozi, askari au viongozi waandamizi wa harakati.
Wafungwa ambao ni viongozi waandamizi katika vyama
vyao nje ya gereza, kila mmoja alifungwa kwenye selo yake iliyokuwa
kwenye jengo B. Wahalifu sugu na wapiganaji wa msituni ambao lengo lao
ni kuuondoa utawala wa makaburu waliwekwa kwenye jengo A ambalo
limetengwa na majengo mengine.
Jengo G limejengwa kwa wafungwa wengi kuishi
katika selo moja. Siku za nyuma wafungwa wenye asili ya Kihindi walikuwa
wakitenganishwa na wafungwa wenye asili ya waafrika weusi.
Mandela siku zote alipopata fursa ya kuzungumza na
askari magereza wa Afrikaner aliwataka kujielekeza kwenye mstari wa
fikira za ANC. Hali hiyo ilimsaidia kujiimarisha kwa kuwa na mbinu mpya
kila mara za kujenga hoja.
Hata hivyo, rafiki wa Mandela, Walter Sisuli
ambaye walikuwa naye gerezani, alichukulia mazungumzo hayo kama mwanzo
wa makubaliano na serikali ya kibaguzi.
Mandela pia akiwa gerezani alitumia muda huo
kujiendeleza katika elimu ya sheria. Alibaini kuwa elimu hiyo inamsaidia
kuweka msingi kwa makubaliano ya mwisho yasiyo ya kumwaga damu, kwa
mslahi ya Afrika Kusini ijayo.
Insha na maandiko ambayo hayakuchapishwa
aliyoyaandika akiwa gerezani yaliifanya Afrika Kusini iwe kama
mshangiliaji, ilionyesha usomi zaidi na uasilia kuliko ule wa awali
wakati wa mapambano na wakoloni. Alikuwa na matarajio ya kupata ukweli.
Mandela aliona jela kama vile maabara ya namna
rangi tofauti zinaweza kuelewana na kuishi kwa utulivu. Aliona gereza
kama mwakilishi wa jamii wa maelewano nchini Afrika Kusini ambayo
yanaweza kudumishwa.
Hata hivyo, mkuu wa gereza Colonel Willie mwaka
1971 alizungumzia uwezo na utayari wa Mandela wa kuongoza serikali ya
mpito nchini Afrika Kusini: “Mandela ana kariba ya kipekee. Amepata
uzoefu wa mabadiliko ya kisiasa. Sidhani kama anasubiri kwa ajili ya
kulipa kisasi. Sijaona chuki kwa yeyote miongoni mwao, lakini Mandela
ana nafasi kubwa ya kuwashawishi.”
Alisema akiwa gerezani amekuwa akishirikiana na
wazungu na wahindi ambapo walimuamini kwa asilimia kubwa, kwakuwa hakuwa
anazungumzia kulipa kisasi kwa watu wa rangi nyingine.
Kilichompeleka jela
Mandela ambaye alikuwa kiongozi wa jumuia ya
African National Congress (ANC), ambayo ilikuwa ikipinga ubaguzi wa
rangi, mwaka 1956 alikamatwa kwa tuhuma za uhaini, lakini aliachiwa
huru. Mwaka 1960 ANC ilipigwa marufuku na Serikali ya Makaburu.
Mwaka 1961, Mandela na viongozi wengine wa ANC waliunda jumuia
nyingine iliyoitwa Umkhonto we Sizwe (MK), ambayo ilikuwa ni kitengo cha
kijeshi cha ANC. Desemba 16, 1961, MK, ambayo Mandela alikuwa mkuu wake
wa majeshi, kilifanya shambulio la bomu kwenye maeneo ya Serikali na
walianzisha mapigano ya msituni. Mandela alikamatwa Agosti 5, 1962, na
alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kuchochea wafanyakazi
kugoma katika mgomo wa wafanyakazi uliotokea mwaka 1961.
Julai 1963 serikali ilishambulia shamba la
Lilliesleaf lililokuwa Rivonia, ambalo lilikuwa likitumiwa na ANC kama
maficho yao. Viongozi 19 wa ANC walikamatwa na kukutwa na nyaraka
zilizoonyesha uhusiano wao na MK na mipango ya kufanya mashambulizi
ikiwemo vita vya msituni.
Serikali ya makaburu iliwafungulia mashitaka
viongozi 11 wa ANC, chini ya sheria ya uhalifu wa kufanya hujuma ya
mwaka 1962. Wakati wa kesi Mandela hakutaka kuwa na shahidi na badala
yake alielezea historia ndefu ya malengo ya ANC na MK, ambapo alikiri
baadhi ya makosa lakini alijitetea kwa kosa la kutumia vurugu kudai
haki. Na Julai 1964 alihukumiwa kifungo cha maisha jela. (NMG).
Comments
Post a Comment