Jamii Forums Wakimbilia Mahakamani....Wadai Kushinikizwa na Jeshi la Polisi Kutoa Siri za Wachangiaji wao
Jamii Forums Wakimbilia Mahakamani....Wadai Kushinikizwa na Jeshi la Polisi Kutoa Siri za Wachangiaji wao
Kampuni ya Jamii Media ambayo ni wamiliki na waendeshaji wa mitandao ya
Jamii Forums na FikraPevu, wamefungua kesi ya Katiba Mahakama Kuu Kanda
ya Dar es Salaam kupinga amri waliyopewa na polisi ya kutoa taarifa
binafsi za wanachama wao.
Akizungumza baada ya kufungua kesi
hiyo jana, Wakili wa Jamii Media, Shukuru Mkwafu alisema lengo lao ni
kutaka Sheria ya Makosa ya Mtandao, kifungu cha 32 na 38 viangaliwe upya
kwani vinasababisha kuvunjwa kwa haki za msingi za Watanzania watumiao
mitandao.
Wakili Mkwafu alisema ili kulinda masilahi ya umma,
lazima vifungu 26(2) na 30(3) vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania vizingatiwe.
Alisema Sheria ya Makosa ya Mtandao Namba
14 ya mwaka 2015, inakiuka haki ya kikatiba namba 16 inayoruhusu kuwapo
na hali ya faragha na kifungu namba 18 kinazungumzia uhuru wa kujieleza.
Mmiliki wa tovuti hizo, Maxence Melo alisema kwa takriban miezi
mitatu iliyopita Polisi imekuwa ikiwashinikiza kwa njia ya barua kutoa
taarifa za baadhi ya wateja wake wanaoonekana kutoa taarifa zile ambazo
kwa namna moja au nyingine, zinaibua ufisadi mkubwa na ukwepaji kodi.
Melo
alisema katika kuhakikisha inasimamia usiri wa wateja wake, wamekuwa
wakihoji sheria inayofuatwa kwenye mashinikizo hayo na kutaka kujua
vifungu vya sheria ambavyo wadau wa mtandao huo wamevivunja, bila kupewa
maelezo yanayoridhisha zaidi ya kuelezwa kuwa hatua zaidi zitachukuliwa
kama hawatatoa ushirikiano kwa Polisi.
Mmoja wa Mawakili
wanaosimamia kesi hiyo itakayotajwa tena Machi 9, Benedict Alex alisema
ni vyema polisi wakaweka wazi mlalamikaji katika madai yao badala ya
kutoa vitisho bila kutoa ufafanuzi.
Comments
Post a Comment