Mheshimiwa Zitto Kabwe Amuomba Rais Magufuli Atengue Agizo la Jakaya Kikwete
Mheshimiwa Zitto Kabwe Amuomba Rais Magufuli Atengue Agizo la Jakaya Kikwete
Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Zitto Kabwe anatafuta nafasi ya kukutana na Rais John Magufuli kumuomba atengue agizo la Rais Jakaya Kikwete la kuzuia ujenzi wa makazi katika Mlima wa Mlole Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Rais
Kikwete alitoa agizo hilo mwaka 2006 kama moja ya hatua za kudhibiti
mmomonyoko wa ardhi na kujaa mchanga kwa bandari ya Kigoma.
Akizungumza
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Kigoma Cinema mjini
Kigoma, Mbunge huyo alisema ameamua kuchukua hatua hiyo kwa kuamini
kwamba taarifa alizopewa Rais Kikwete zilizosababisha kutoa agizo hilo
hazikuwa sahihi.
Zitto
alisema Rais Kikwete alipewa taarifa potofu kwamba mmomonyoko wa udongo
kutoka katika eneo hilo ndiyo unaosababisha kujaza mchanga na kupunguza
kina katika bandari ya Kigoma.
Mbunge
huyo wa Kigoma Mjini alisema kuwa tafiti zilizofanyika na taarifa
zilizopo zinaonesha kuwa kupanuliwa kwa Mto Lukuga kunafanya maji kutoka
kwa wingi na kuingia bahari ya Atlantiki ndiko kulikochangia kupunguza
kina cha maji katika maeneo mbalimbali ya mwambao wa Ziwa Tanganyika.
Kwa
mujibu wa tathmini iliyofanywa mwaka 2008 inaonyesha kuwa kiasi cha Sh
bilioni tano kilikuwa kikihitajika kwa ajili ya kuwalipa fidia wakazi
hao, fedha ambazo uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji
imesema haiwezi kuzilipa hivyo kutaka mamlaka za serikali kuona namna ya
kutafuta fedha hizo na kugharamia kuwalipa watu hao.
Wakizungumzia
kauli ya Zitto, baadhi ya wakazi wa eneo la Mlole ambao wameathirika
kwa kiasi kikubwa na agizo hilo la Rais Kikwete, walisema kuwa wameanza
kupata matumaini ya kuona thamani ya nyumba zao kwani tangu kutolewa kwa
agizo hilo nyumba zao zimekuwa hazina thamani mahali popote.
Comments
Post a Comment