Mkuu Wa Majeshi Aongoza Kuwaaga Maofisa Majenerali 16 Wa Jwtz Waliostaafu
Mkuu Wa Majeshi Aongoza Kuwaaga Maofisa Majenerali 16 Wa Jwtz Waliostaafu
MKUU
wa Majeshi Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange amewaongoza wanajeshi
mbalimbali kuwaaga Majenerali 16 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania
(JWTZ) ambao wamemaliza muda wa utumishi wao.
Sherehe
hizo zilifanyika Uwanja wa Kambi ya Jeshi wa Twalipo, Mgulani jijini
Dar es Salaam kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 6:30 mchana. Sherehe
hizo ziliongozwa na bendi ya jeshi na gwaride maalumu.
Miongoni
mwa waliomaliza muda wao ni Meja Jenerali Samuel Ndomba ambaye aliwahi
kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mkuu
wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na hadi anastaafu alikuwa Mnadhimu Mkuu
wa JWTZ.
Wengine
ni Luteni Jenerali Paul Mella ambaye alikuwa Kamanda wa Majeshi ya
Kulinda Amani ya Darfur, Sudan na Brigedia Jenerali Harold Mziray ambaye
alikuwa Mkuu wa Shule ya Infantria, Arusha.
Majenerali
wengine walioagwa ni Brigedia Jenerali Martin Mwankanye aliyekuwa
Mkurugenzi wa Mahusiano ya Kimataifa jeshini, Brigedia Jenerali John
Chacha aliyekuwa Kamanda wa Brigedi ya Tembo na Brigedia Jenerali Ezra
Ngingwango aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Ndege na Usafirishaji jeshini.
Brigedia
Jenerali Mrisho Abdallah aliyekuwa Mratibu Miradi ya Maendeleo jeshini
naye ameagwa kama ilivyo kwa Brigedia Jenerali Emmanuel Maganga
aliyekuwa Mkuu, Tawi la Ukaguzi jeshini, Brigedia Augustino Gailanga
aliyekuwa Mkuu wa Tawi Jeshi la Akiba, Brigedia Jenerali Luhindi Msangi
aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Tiba Lugalo, Dar es Salaam na Meja
Jenerali Raphael Muhuga wa JKT.
Wengine
ni Meja Jenerali Charles Muzanila aliyekuwa Mkuu wa Shirika la Mzinga
Morogoro, Meja Jenerali Ezekiel Kyunga aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha
Ukamanda na Unadhimu kilichopo Duluti mkoani Arusha, Meja Jenerali
Joseph Kapwani aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Anga, Meja Jenerali Vincent
Mritaba aliyekuwa Mkuu wa Utumishi jeshini na Meja Jenerali Salum Kijuu,
Mkuu wa Jeshi la Nchi Kavu.
Brigedia
Jenerali mstaafu, Msangi (kulia mbele), akikagua gwaride maalumu
waliloandaliwa maofisa hao wastafu wakati wakiagwa rasmi baada ya
kumaliza utumishi wao jeshini.
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), mstaafu Meja Jenerali, Raphael Muhuga, akikagua gwaride hilo.
Mkuu
wa Majeshi, Jenerali, Davis Mwamunyange (kushoto), akisalimiana na
kumpongeza Mkuu wa Vikosi vya Kulinda Amani Umoja wa Mataifa, Luteni
Jenerali mstaafu, Paul Ignas Meela katika hafla hiyo.
Comments
Post a Comment